Monday 1 January 2018

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein: Kinga ni bora kuliko tiba

 Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa  katika maadhimisho ya siku ya mazoezi Kitaifa yaliyovishirikisha vikundi mbali mbali vya mazoezi kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara pamoja na vikosi vya SMZ yaliyoanzia katika uwanja wa Tumbaku na kuishia katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar yaliosimamiwa na Chama Cha Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA).
Viongozi mbali  mbali walishiriki katika maadhimisho hayo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi wengine wa Seriali na vyama vya siasa na wananchi ambapo katika maelezo yake Dk. Shein alisisitiza kuwa kufanya mazoezi kunasaidia kupunguza uzito wa mwili na kuwataka wananchi kufanya mazoezi na kutosubiri hadi wakaambiwa na daktari.
Dk. Shein aliwasisitiza wananchi kuzingatia usemi maarufu wa mabingwa wa lugha ya kiswahili kwamba “Tahadhari kabla ya athari” na “Kinga ni bora kuliko tiba”, hivyo alisisitiza ni vyema kila mmoja akajiwekea muda maalum wa kufanya mazoezi yanayolingana na afya na umri wake.
Pia, Dk. Shein alitangaza rasmin kuwa maadhimisho hayo ya Siku ya Mazoezi Kitaifa hapo mwakani yatafanyika Kisiwani Pemba huku akiitaka Wizara ya Habari,  Utalii, Utamaduni na Michezo kukitafutia ofisi Chama Cha Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA) ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.

No comments:

THIS BLOG DESIGNED BY

HOME BOYZ GRAPHICS LABORATORY